Monday, November 11, 2013

Rekodi ya ufungaji yapanda Ligi Kuu

Kikosi cha Simba
Na Abducado Emmanuel, Dar es Salaam

CHATI ya ufungaji mabao katika Ligi Kuu ya Vodacom, imeonekana kupanda kwa kasi msimu huu kutokana na mabao 207 kufungwa hadi kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo tofauti na msimu uliopita.

Msimu uliopita baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, jumla ya mabao 196 yalifungwa lakini msimu huu kuna tofauti kubwa kutokana na idadi ya mabao yaliyofungwa.

Timu za Simba, Mtibwa Sugar na Yanga ndizo zimepata ushindi mnono katika ligi hiyo, baada ya Simba kuifunga Mgambo Shooting mabao 6-0, Mtibwa Sugar iliifunga JKT Oljoro mabao 5-2, huku Yanga ikiifunga Ashanti United mabao 5-1.

Yanga ndiyo inayoongoza kwa kufunga mabao mengi ikiwa imefunga mabao 31, Simba inafuatia kwa mabao 26 na Azam FC imefunga 23, huku Mgambo JKT ndio timu iliyofunga mabao machache kwa kupachika wavuni mabao matatu.

Mshambuliaji wa Simba, Amisi Tambwe anaongoza kwa kufunga jumla ya mabao 10 akifuatiwa na Elias Maguri wa Ruvu Shooting aliyepachika mabao tisa. Hamis Kiiza (Yanga), Kipre Tchetche (Azam FC) na Juma Luizio (Mtibwa Sugar) kila moja amepachika mabao nane.

Kiiza amefikia rekodi yake ya msimu uliopita, baada ya kufunga mabao nane aliyofunga.

Tanzanite yatua Dar kuivutia kasi Afrika Kusini

Timu ya Taifa Wanawake walio chini ya umri wa miaka 20 (Tanzanite)
Na John Dande, Dar es Salaam:     

TIMU ya Taifa ya Wanawake walio chini ya umri wa miaka 20 (Tanzanite), imefuzu kucheza raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Dunia kwa ushindi wa jumla ya mabao 15-1, baada ya juzi kuinyuka Msumbiji mabao 5-1.

Mabao ya Tanzanite katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Zimpeto jijini Maputo, yalifungwa na Sherida Boniface aliyepachika matatu (hat trick) wakati mengine yalifungwa na Vumilia Maarifa na Donesia Minja.

Msafara wa Tanzanite ulioongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao uliwasili jana alasiri Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Akizungumza baada ya kuwasili nchini jana, kocha mkuu wa timu hiyo, Rogasian Kaijage alisema mechi ilikuwa ngumu lakini kwa sasa wanajipanga kuikabili Afrika Kusini katika mechi itakayochezwa kati ya Desemba 6 na 8 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Uchaguzi Mkuu TBF Desemba 10

Na Mohamed Mharizo, Dar es Salaam:

UCHAGUZI mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), unatarajia kufanyika Desemba 10 mwaka huu jijini Mbeya.

Kwa mujibu wa Rais wa TBF, Mussa Mziya, uchaguzi huo unafanyika kwa mujibu wa katiba baada ya uongozi uliopo madarakani kumaliza muda wake.

“Napenda kuchukua fursa hii kutoa tangazo rasmi la tukio la uchaguzi mkuu wa viongozi wa TBF utakaofanyika Desemba 10 mwaka huu jijini Mbeya na kikatiba inabidi ufanyike uchaguzi kuwapata viongozi wapya watakaoendesha shughuli za shirikisho kwa miaka minne ijayo,” alisema.

Alisema uchaguzi huo utafanyika baada ya kumalizika kwa mashindano ya Taifa Cup, ambayo mwaka huu yanafanyika mkoani Mbeya kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 8 jijini Mbeya.

Alizitaja nafasi zitakazowania katika uchaguzi huo ni Rais, Makamu wa Rais, Katibu Mkuu, Katibu Mkuu Msaidizi, Mhazini, Kamishna wa Mipango, Kamishna wa Ufundi na Mashindano, Kamishna wa Waalimu, Kamishna wa Watoto na Shule, Kamishna wa Wanawake, Kamishna wa Waamuzi, Kamishna wa Tiba ya Wanamichezo na Kamishna wa Walemavu.

Alisema taratibu zote za uchaguzi huo zitasimamiwa na Baraza la Michezo la Tanzania (BMT) ambao ndio watakaokuwa wakitoa fomu za maombi ya wagombea.

“Kwa niaba ya uongozi wa shirikisho napenda kuchukua nafasi hii kuwaomba wadau, wapenzi wa michezo na wananchi wote kwa ujumla wenye sifa na wanaopenda kuongoza wajitokeze kwa wingi kuchukua fomu za maombi ya uongozi, baada ya tangazo la BMT la kuanza kuchukua fomu hizo kwa nafasi zote zilizotangazwa,” alisema.